KIGAMBONI WAKABIDHIWA MRADI WA MAJI

Jitihada za serikali na wadau wa maendeleo kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kijamii zimeendelea kuzaa matunda baada ya leo taasisi ya kiislam ya Dhi Nureyn yenye makao yake makuu mkoani Iringa, kukabidhi mradi wa kisima cha maji kwa wakazi wa mtaa wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kukamilika kwa mradi huo ni matokeo ya maombi ya Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Hashim Mgandila kwa taasisi hiyo, ambayo tayari imechimba jumla ya visima 180 katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliohudhuriwa na diwani wa kata ya Kigamboni Doto Msawa, Mwakilishi wa Dhi Nureyn Islamic Foundation Muzamil Issa pamoja na Msimamizi wa miradi ya maji Ali Mussa Upete wamesisitiza umuhimu wa miradi ya aina hiyo kutunzwa ili iwanufaishe wananchi kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa risala iliyomwa kwenye uzinduzi huo, mradi huo ulianza mwanzoni mwa mwaka 2016, ambapo tangu wakati huo kamati ya uendeshaji imefanikiwa kuongeza idadi ya wateja na makusanyo ya fedha za mradi kutoka shilingi laki nne na mia tisa hadi kufikia Shilingi milioni 10 na laki nne.



No comments